Naibu Wa Rais Rigathi Gachagua hii leo aliongoza katika zoezi la upokezi wa shehena ya kwanza ya Mafuta yaliyoagizwa na kununuliwa katika ushirikiano kati ya serikali ya Kenya na ile ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE)
Mkataba huo wa kibiashara ulifuatia makubaliano ambayo yatashuhudia kampuni ya kitaifa ya usambazaji mafuta ya Abu Dhabi ADNOC ikiwa mmoja wasambazaji wa mafuta humu nchini kwa kipindi cha miezi tisa. Meli mbili zilizowasili bandarini Mombasa hii leo zilikuwa zimepakia tani 172,191 za petroli, dizeli na mafuta ya ndege.
Naibu wa rais aliyeandamana na Waziri wa kawi nchini Davis Chirchir, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir Pamoja na mwenyekiti wa mamlaka ya bandari nchini Benjamin Tayari, alieleza kwamba serikali imeweka mipango kabambe ya kuhakikisha kwamba usambazaji wa mafuta hautatatizika chini ya makubaliano haya mapya.