Taifa la Kenya jana jioni lilishuhudia historia baada ya bunge la kitaifa kwa mara ya kwanza kumng’atua mamlakani naibu wa rais.
Baada ya kujadiliwa kwa hoja ya kumtimua Rigathi Gachagua na yeye kuwasilisha ushahidi wake bungeni, wabunge 281 walipiga kura kuunga mkono hoja hiyo iliyowasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.
Mutuse aliwasilisha mashtaka 11 dhidi ya Gachagua kwenye hoja yake ikiwa ni pamoja na kueneza semi za chuki na kujilimbikizia mali kwa njia ya kutilia shaka. Aidha Wabunge 44 walipiga kura ya kupinga hoja hiyo iliyozua mjadala mkali bungeni.
Ni mbunge mmoja aliyejizuia kupiga kura huku baadhi ya wabunge ambao awali walikuwa wametia saini hoja hiyo wakiamua kutohudhuria kikao hicho.
Kufuatia kupitishwa kwa hoja ya kumtimua Gachagua madarakani, Spika wa Bunge la kitaifa Moses Wetang’ula sasa atahitajika kumtaarifu Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi kuhusiana na uamuzi wa Bunge la Taifa.
Kisha Kingi anatarajiwa kuitisha kikao cha Maseneta kuangazia uamuzi wa Bunge la kitaifa.Ikiwa Seneti itakubaliana nao, basi Gachagua atavuliwa wadhifa wa Naibu Rais.
Hata hivyo, katika hali kama hiyo, Gachagua anaweza kuelekea mahakamani na kupata agizo la kuzuia kuondolewa kwake madarakani.