Wasafiri kutoka pembe tofauti za taifa watalazimika kugharamika hata zaidi katika usafiri wao kuanzia kesho, kwani nauli ya usafiri kuelekea maeneo mbalimbali ya taifa inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 30.

Hatua hii imefuatia agizo la mwenyekiti wa Wamiliki wa Matatu nchini, Bwana Albert Karakacha, ambaye ametoa mwongozo kwa wahudumu wa usafiri wa umma kuongeza nauli kufuatia kuongezeka kwa bei ya mafuta.

Katika kikao na waandishi wa habari mapema leo, Bwana Karakacha alisema kuwa hatua ya kuongezwa kwa nauli ni njia pekee ya kuwalinda wawekezaji katika sekta ya usafiri na kuhakikisha kuwa wamiliki Matatu nchini wataweza kukabiliana na gharama ya juu ya maisha. Kwa mujibu wa taarifa yake, bei za usafiri kwenda miji mbalimbali nchini zinatarajiwa kuongezeka kwa kati ya shilingi 100 na 300, huku nauli za usafiri ndani ya miji zikitarajiwa kupanda kwa kati ya shilingi 10 na 70.

Ongezeko hili la nauli limejiri baada ya bei ya mafuta kuongezeka kwa baada ya kuidhinishwa kwa mswada wa fedha wa mwaka 2023, jambo lililoibua hisia mseto kutoka kwa wakenya katika pembe tofauti za taifa. Ongezeko hili la nauli linatarajiwa kuendelea kuwa mzigo mzito zaidi kwa wananchi wanaotumia usafiri wa umma.

July 4, 2023