Wambui Nyutu NCIC

Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) imetoa ripoti inayobainisha kuongezeka kwa kiwango cha uajiri kwa misingi ya kikabila katika serikali za kaunti nchini. Ripoti hiyo inasisitiza kuwa hali hii imeongezeka, hasa katika serikali za kaunti zilizoingia madarakani mwaka jana, ikilinganishwa na serikali za hapo awali.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na NCIC, kaunti 36 kati ya 47 zimeshuhudia ongezeko la uajiri wa watu kutoka kabila moja, hali inayozua wasiwasi kuhusu utangamano na usawa wa nafasi za ajira katika utumishi wa umma. Kaunti ya Nairobi imeonekana kuwa na mafanikio katika kuwahusisha watu kutoka makabila mbalimbali.

Ripoti hiyo pia imebainisha kuwa kuna kabila 29 ambazo zimetengewa asilimia moja pekee ya nyadhifa za utumishi wa umma katika kaunti mbalimbali.

Kwa ujumla, jamii ya Kalenjin inaongoza kwa idadi kubwa ya ajira katika sekta ya utumishi wa umma, ikiwa na asilimia 15.83 ya wafanyakazi wote 184,876 katika kaunti mbalimbali. Jamii ya Kikuyu ina asilimia 15.77 ya wafanyakazi, na Jamii ya Luhya ina asilimia 11.6.

SOMA PIA: Tume ya NCIC yataka kusitishwa kwa maandamano

Kamishna wa NCIC, Abdulaziz Ali Farah, amesema kuwa ripoti hiyo inatoa mwongozo kuhusu usawa katika utumishi wa umma kwenye serikali za kaunti, miaka kumi tangu kuanzishwa kwa serikali za ugatuzi nchini.

 

November 17, 2023