BY ISAYA BURUGU,03,NOV,2022-Naibu chanzela wa chuo kikuu cha Kenyatta Profesa Paul Wainaina amerejea chuoni humo hivi leo na kulakiwa kwa shangwe na nderemo kutoka kwa wanafunzi na wahadhiri.

Hii ni baada yake kuachishwa kazi mwezi Julai  mwaka huu kufuatia msimamo wake kuhusu ardhi ya chuo kikuu hicho.

Aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta alitofautiana vikali na profesa Wainaina kuhusu ardhi ya chuo hicho baada ya Uhuru kumuagiza naibu huyo wa chanzela kukabidhi stakabadhi za umiliki wa ardhi ya chuo hicho kwa serikali ili kufanikisha mpango wa kutumia sehemu ya ardhi ya chuo kwa miradi kadhaa ya uwekezaji.

Hata hivyo Wainaina alipinga wazo hilo na kushikilia kuwa ardhi ya chuo inapaswa kusalia ilivyo na kutumiwa kwa maswala yanayohusiana na chuo pekee.

Ni hali iliyozua mzozo kati ya serikali na wanafunzi chuoni humo huku wanafunzi wakimuunga mkono Profesa Wainaina na kupinga kuachishwa kwake kazi kwa msimamo huo wake.Hata hivyo akizungumza hivi leo aliporejea chuoni Naibu chanzela huyo amerejelea msimamo wake kuwa atazidi kutetea ardhi ya chou hicho sawa na mali nyingine.

 

November 3, 2022