Waziri wa Uchukuzi nchini, Kipchumba Murkomen, ameiagiza Mamlaka ya Trafiki na usalama barabarani (NTSA) kuanzisha msako dhidi ya magari ya kibinafsi yanayojihusisha na uchukuzi wa umma bila kibali.

Akizungumza siku ya Alhamisi katika mkutano na wamiliki wa matatu nchini ulioandaliwa katika ukumbi wa KICC Jijini Nairobi, Murkomen amesisitiza umuhimu wa kurejesha utaratibu na nidhamu katika sekta ya uchukuzi.

Magari aina ya Toyota Sienta, Probox, Voxy, na Sienna yametajwa kuwa sugu katika uchukuzi wa umma bila kibali. Waziri ameagiza msako huo kuanza mara moja asubuhi ya Ijumaa, tarehe 1 Desemba 2023.

Wamiliki wa magari yanayoshiriki katika uchukuzi wa umma pia wametakiwa kuhakikisha kwamba magari yao yamesajiliwa na chama cha wamiliki wa matatu nchini. Waziri Murkomen amesisitiza kuwa hatua hii ni muhimu itasaidia pakubwa katika mipango ya serikali ya kurejesha nidhamu katika sekta ya uchukuzi.

 

 

 

November 30, 2023