NTSA-CARS

Huku shule zikielekea kufungwa juma lijalo, Mamlaka ya Trafiki na Usalama Barabarani (NTSA) imechukua hatua za tahadhari kwa madereva na wachukuzi wengine wa umma dhidi ya kuvunja sheria za trafiki na utovu wa nidhamu barabarani. Hatua hii inalenga kuhakikisha usalama wa wanafunzi na umma kwa ujumla wakati wakisafiri kuelekea nyumbani kwa likizo.

Meneja wa Mikakati ya Usalama Barabarani wa NTSA, Bw. Samwel Musumba, aliweka wazi kuwa matatu zote zitakazopatikana zikijihusisha na visa vya utovu wa nidhamu zitakabiliwa na sheria kali za trafiki. Pia, aliongeza kuwa NTSA inasikitika sana na visa kadhaa ambapo wanafunzi wa shule hujihusisha katika matumizi ya mihadarati katika magari ya uchukuzi wa umma.

Kufuatia hofu ya usalama wa wanafunzi hasa wale wanaosafiri mwendo mrefu, Meneja huyo wa pia aliwashauri wasimamizi wa shule mbalimbali kuwaruhusu wanafunzi kuondoka shuleni mapema wakati wa kufunga shule. Hii itawapa wanafunzi nafasi ya kufika nyumbani kwa wakati unaofaa na kupunguza hatari ya kukumbana na changamoto za kiusalama wakati wa safari.

August 4, 2023