Kinara wa upinzani Raila Odinga amewataka Wakenya kujihusisha katika msururu wa shughuli za uasi kama njia ya kupinga mipango ya Serikali kuwatoza ushuru zaidi na kuendeleza kile alichokitaja kama usaliti mjini kwa kuwatoza Wakenya ushuru bila idhini yao.
Katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa leo na mrengo wa Upinzani katika uwanja wa Kamukunji, Odinga, ambaye amerejea nchini hii leo, amesisitiza kuwa Wakenya wamechoka kuhangaishwa na Serikali ya Kenya kwanza. Amewahimiza kusimama kidete na kupinga unyanyasaji zaidi. Aidha, Odinga amekataa kuingia katika meza ya mazungumzo na Serikali huku pia akitangaza kuwa viongozi wa Upinzani watarudi kwa maandamano ya kitaifa tarehe saba mwezi ujao.
Tuliwaambia punda amechoka. Hawakutuskiza. Wamezidi kuwekelea mizigo punda mgongoni. Sasa wakati umefika punda sasa awapige mateke. Ruto haelewi, lakini tutamuonesha, tutamfunza. Tuanze Kazi!!! pic.twitter.com/56wRaCnqu8
— Raila Odinga (@RailaOdinga) June 27, 2023
Wakati hayo yakijiri, viongozi wa Kenya Kwanza ambao walikuwa wakiongoza mazungumzo ya pande mbili kati ya Serikali na Upinzani, wametoa mwaliko kwa viongozi wa Upinzani kurejea katika meza ya mazungumzo tarehe 4 mwezi ujao ili kutatua suala la uteuzi wa makamishna wa tume ya uchaguzi na uratibu wa mipaka nchini IEBC.
George Murugara, Mwenyekiti Mwenza wa mazungumzo hayo, amesisitiza umuhimu wa kurejea kwenye mazungumzo hayo baada ya kukamilika kwa shughuli nzima ya bajeti iliyokamilika juma lililopita. Hata hivyo, upinzani umetoa jibu la kukataa kushiriki katika mazungumzo ya aina hiyo.