Ofisi ya Gavana wa Kisii Simba Arati ilizingirwa na maafisa wa kitengo cha GSU mapema hii leo ambapo gavana huyo alizuiliwa kuingia ofisni mwake. Akizungumza na waandishi wa habari, gavana huyo alielezea wasiwasi wake akidai kuwa hiyo ni njama kumkamata.
Alitaja uwezekano wa kukamatwa kwake kutokana na kuunga mkono chama cha ushirika cha bodaboda na kujitolea kwake katika kupambana na ufisadi katika kaunti hiyo.Pia alikashifu kufungwa kwa ghafla kwa afisi za chama hicho cha Bodaboda kwa madai kuwa kinawafadhili wahalifu.
Tukio hilo linafuatia ufichuzi wa Arati kwamba alipokea taarifa za kijasusi zinazopendekeza uvamizi wa usiku kwenye makazi yake. Hata hivyo alisema kuwa alivitaka vikosi vya usalama kufanya uvamizi wowote wakati wa mchana.
Akiongezea kufadhaika kwake, Arati alielezea kusikitishwa na ukosefu wa mawasiliano ya uwazi kutoka kwa maafisa wakuu wa usalama wa kaunti, akiwemo Kamishna wa Kaunti Tom Anjere, kuhusiana na madhumuni ya maafisa hao wa GSU kuwepo katika afisi zake.