Papa Mtakatifu Francisko amemteua padre Cleophas Oseso Tuka, kama Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Nakuru.
Taarifa za Uteuzi wa padre Oseso zilichapishwa rasmi katika gazeti la Vatican la L’Osservatore Romano mnamo tarehe 15 Februari 2023 saa 12.00 adhuhuri kwa saa za Roma na saa 2.00 adhuhuri kwa saa za Kenya.
Mwakilishi wa papa nchini Kenya na Sudan Kusini, Askofu Mkuu Bert van Megen, pia alituma mawasiliano rasmi kwa Baraza la Maaskofu Katoliki KCCB.
Askofu Mteule Oseso amekuwa akihudumu kama vicar jenerali wa Jimbo Katoliki la Nakuru tangu tarehe 25 Machi 2019 alipoteuliwa na aliyekuwa Askofu wa Nakuru na ambaye sasa ni Askofu Mkuu wa Kisumu, askofu Maurice Muhatia Makumba.
Askofu mteule alizaliwa mwaka wa 1967 huko Naivasha. Alienda katika Seminari ya St. Mary’s Molo kwa masomo yake ya kiroho na kisha akakwenda Seminari Kuu ya Mtakatifu Agustino Mabanga kusomea falsafa na baadaye Seminari kuu ya Mtakatifu Mathias Mulumba Tindinyo kwa masomo yake ya theolojia.
Alitawazwa kuwa kasisi wa Dayosisi ya Nakuru mwaka wa 1995. Baada ya kutawazwa, aliwekwa wakfu katika Parokia ya Holy Cross, Shabaab, kisha akaenda kusomea masuala ya fedha katika Chuo cha Mwangaza wakati huo mwaka wa 1996.
Hadi kuteuliwa kwake, Askofu Mteule alikuwa akihudumu kama paroko wa Parokia ya Bahati.