VATICAN CITY – Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Francis, mwenye umri wa miaka 88, ameruhusiwa kuondoka Hospitali ya Gemelli mjini Roma baada ya kulazwa kwa zaidi ya wiki tano kutokana na matatizo ya kupumua. Madaktari wamesema atahitaji angalau miezi miwili ya kupumzika katika makazi yake Vatican.
Hali Yake Wakati wa Matibabu
Kwa mujibu wa Dkt. Sergio Alfieri, mmoja wa madaktari waliomhudumia Papa, kiongozi huyo alikumbwa na hali mbili hatari zilizohatarisha maisha yake wakati wa matibabu. Hata hivyo, hakuwahi kulazwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) wala kutiwa mipira ya oksijeni, na alibaki macho na mwenye ufahamu wakati wote wa matibabu.
Ingawa bado hajapona kabisa, madaktari wamesema hana tena nimonia. Ikiwa hali yake itaendelea kuimarika, ataweza kurejea kazini hivi karibuni.
Mapokezi ya Waumini
Baada ya kuondoka hospitalini, Papa alitokea akiwa kwenye kiti cha magurudumu. Alitabasamu, akapunga mkono, na kuwapa waumini ishara ya dole gumba (thumbs up). Mamia ya waumini walikusanyika nje ya hospitali wakimwita kwa shangwe, wakisema “Francis, Francis, Francis.”
SOMA PIA: Papa Francis Asema Hana Nia ya Kujiuzulu Kutokana na Afya Njema
Papa Francis alikuwa ameonekana hadharani mara moja tu tangu alazwe. Vatican ilitoa picha wiki iliyopita ikimuonyesha akisali katika kanisa la hospitali. Kwa sasa, ataendelea kupumzika Vatican hadi madaktari watakaporidhika kuwa anaweza kurejea katika majukumu yake kikamilifu.