Polisi katika kaunti ya Baringo wamemkamata mshukiwa wa ujambazi huko Kapedo Akoret, Kaunti Ndogo ya Tiaty na kupata bunduki mbili na risasi 15.

Kulingana na polisi katika eneo hilo, Lonyangapat Amerinyang’ amekuwa akifuatiliwa na polisi kwa miaka minne iliyopita na wanashuku kuwa ndiye mhusika mkuu wa visa vya ujambazi katika eneo la Kaskazini mwa bonde la Ufa.

Kukamatwa kwa Lonyangapat kunaleta jumla ya idadi ya majambazi ambao wamekamatwa huko Baringo kuwa watatu. Akithibitisha kukamatwa kwa mshukiwa huyo, Kamanda wa Polisi wa Baringo Julius Kiragu amesema kuwa kukamatwa kwa watu hao ni hatua kubwa katika vita dhidi ya ujambazi.

Kwa upande wake Kamishna wa kaunti ya Baringo Stephen Kutwa amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na polisi kukabiliana na ujambazi. Alisema taarifa kutoka kwa wananchi ni muhimu katika kuwabaini na kuwakamata majambazi.

Kaunti ya Baringo imekuwa ikikumbwa na msururu wa mashambulizi ya ujambazi huku lile la hivi punde likiwa jana ambapo Askari mmoja wa Polisi wa Akiba alijeruhiwa vibaya katika eneo la Ng’aratuko huko Baringo Kaskazini.

Kukamatwa kwa Amerinyang’ kunakuja huku serikali ikizidisha juhudi zake za kupambana na ujambazi katika eneo la North Rift.

November 16, 2023