Biashara ya Pombe haramu Mlima Kenya

Maafisa wa usalama katika ukanda wa Mt. Kenya wameshutumiwa kwa utepetevu katika jitihada za kukabiliana na biashara ya pombe haramu. Kauli hii imetolewa na viongozi mbalimbali wa ukanda wa mlima Kenya, wakiongozwa na Naibu wa Rais Rigathi Gachagua.

Wakizungumza katika Shule ya Msingi ya Kangai, Mwea, kaunti ya Kirinyaga wakati wa hafla ya mazishi ya watu 17 waliopoteza maisha yao baada ya kunywa pombe haramu, viongozi hao wameilaumu idara ya mahakama, maafisa wa utawala, na tume ya huduma za polisi nchini, kwa kushirikiana na wafanyabiashara wanaoendeleza biashara ya uuzaji wa pombe haramu.

SOMA PIA : Vita dhidi ya Pombe Haramu na mihadarati vyashika kasi Narok.

Naibu wa Rais pia ametoa wito kwa viongozi wachanga katika eneo la Mlima Kenya kujiepusha na siasa za mara kwa mara na badala yake kushiriki katika mapambano dhidi ya biashara hii ya pombe harmu katika eneo hilo.

Wakati haya yakijiri, Gavana wa Kirinyaga, Ann Waiguru, ameamuru kufungwa mara moja kwa baa na maduka mengine yanayouza vileo katika Kaunti ya Kirinyaga. Gavana huyo ametangaza kuanzisha upya mchakato wa utoaji leseni kwa wamiliki na wauzaji wa vileo katika kaunti hiyo. Gavana Waiguru ameeleza kwamba tatizo la biashara ya pombe haramu limekuwa kubwa katika kaunti hiyo, na limeleta mateso kwa wananchi kutokana na watu wanaotafuta faida kwa njia haramu.

 

February 17, 2024