Idara ya Polisi nchini imetangaza kupiga marufuku shughuli za maandamano katikati mwa jiji la Nairobi. Kaimu Inspekta Generali wa Polisi, Douglas Kanja, alitoa tangazo hilo kupitia taarifa rasmi siku ya Jumatano. Kanja alieleza kuwa maafisa wa polisi wamekuwa na wakati mgumu katika kudhibiti waandamanaji na kuhakikisha usalama wao.
Katika taarifa hiyo, NPS ilieleza kwamba maandamano hayo yameingiliwa na watu wenye nia ya kutekeleza uhalifu. Vilevile imeeleza kwamba maandamano ya Gen Z hayana viongozi, hivyo basi hakuna watu wa kutoa mwelekeo ili kuhakikisha kwamba yanaendelea kwa njia ya amani.
PRESS RELEASE ON PLANNED DEMONSTRATIONS BY KENYAN YOUTHS ON JULY 18, 2024 pic.twitter.com/zo6eTGfdCD
— National Police Service-Kenya (@NPSOfficial_KE) July 17, 2024
Vijana wamekuwa wakiandamana kuanzia tarehe 18 mwezi jana wakipinga mswada wa fedha uliofutiliwa mbali, baada ya waandamanaji hao kupenyeza kwenye bunge. Maandamano hayo yameonekana kufuata mkondo wa kuitisha mageuzi ya serikali yaliyomlazimu rais kulivunja baraza la mawaziri.
SOMA PIA: Rais William Ruto alivunja baraza lake la mawaziri katika mabadiliko ya hivi punde.
Asubuhi ya leo, Idadi kubwa ya maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia imeshika doria katikati mwa jiji la Nairobi, kwa lengo la kudhibiti maandamano ya vijana wa Gen Z. Maafisa zaidi wameweka kambi katika bustani ya Uhuru Park, ambapo vijana hao walipanga kukongamana leo.
Hata hivyo, uamuzi huu umepokea pingamizi mitandaoni, ambapo wananchi wamehoji uhalali wa kuingilia uhuru wa kuandamana uliowekwa kwenye katiba.