Azimio maandamano

Kinara wa upinzani Raila Odinga amesema kwamba maandamano ya upinzani yaliyositishwa yatarejelewa tena katika kipindi cha juma moja lijalo.

Akizungumza katika jengo la Ufungamano baada ya kuongoza mkutano wa mashauriano na wananchi, Odinga amesema kwamba atatangaza tarehe rasmi ya kurejea kwa maandamano hayo, baada ya kukamilika kwa kipindi cha Ramadhan, akisema kwamba muungano wake utaendelea na mazungumzo ya pande mbili iwapo yataandaliwa nje ya bunge, huku akiongeza kwamba maandamno hayo ni ya kushinikiza serikali kuyapa kipaumbele mambo yanayomhusu mwananchi wa kawaida.

Aidha aliikashifu serikali kwa kutoyazingatia maoni ya pande tofauti kabla ya kufanya na kutoa maamuzi.Tangazo la Odinga lilikujia saa chache baada ya muungano huo kukata kuongezwa kwa idadi ya viongozi watakaoshiriki katika mazungumzo ya pande mbili kati ya upinzani na serikali.

Jopo la watu saba lililoteuliwa na muungano wa Azimio la Umoja kuwakilisha kwenye mazungumzo ya pande mbili, liliongeza wanachama wengine watatu katika kikosi chao, huku likiwataja wakili Paul Mwangi, Prof Makau Mutua na Jeremiah Kioni kama wanachama wengine wasikuwa bungeni na ambao pia watakaohusika katika shughuli za jopo hilo.

Mwenyekiti wa jopo hilo Otiende Amollo alitangaza kuwa tayari wamebuni rasimu ya mpango utakaosaidia kuyaelekeza mazungumzo hayo pindi yatakapoanza. Aidha alipinga uteuzi wa mbunge wa Eldas Aden Keynan kwenye timu ya kenya kwanza akidai kuwa ni mbunge aliye chini ya muungano wa azimio la umoja.

April 13, 2023