Rais William Ruto, ameagiza idara za usalama nchini, kuwapa kipaumbele wananchi waliohudumu katika idara ya huduma ya kitaifa ya vijana (NYS). Kulingana na agizo hilo, asilimia 80 ya makurutu wote watakaochukuliwa katika idara za Polisi, Jeshi, maafisa wa kulinda misitu na wale wa kuwalinda wanyamapori, watakua vijana waliohudumu katika NYS.
Rais Ruto alitoa agizo hili katika hotba yake kuhusu Mustakabali wa taifa siku ya Alhamisi, akiongeza kwamba lazima kila kijiji na wadi iweze kuwa na wawakilishi katika zoezi la kuwachagua makurutu. Agizo hili linakuja wakati serikali inalenga kuongeza idadi ya wakenya wanaojiunga na idara ya NYS, ikiwa na lengo la kuwafikia wakenya elfu 40 mwaka ujao.
Rais Ruto amesisitiza umuhimu wa kutoa kipaumbele kwa wale waliohudumu kwenye NYS, akiashiria imani yake katika uwezo wao wa kuleta mabadiliko chanya katika idara za usalama.
Waziri wa Utumishi wa Umma, Moses Kuria, amekuwa mstari wa mbele kuunga kwake mkono agizo la rais, huku akisema kwamba vijana waliohudumu kwenye NYS watatumia muda mfupi kwenye mafunzo maalum ya asasi za usalama, na hivyo kupunguza matumizi ya serikali kwa kiasi kikubwa.