MAKAZI

Rais William Ruto ametoa wito kwa serikali za Afrika kuelekeza juhudi zao kwenye mipango ya kuboresha makazi ya wananchi wao, hasa wale wanaoishi katika vitongoji duni.

Katika hotuba yake siku ya tatu ya kongamano la Hali ya Anga barani Afrika, Rais Ruto amesisitiza umuhimu wa viongozi kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha wananchi wanapata makaazi bora, hususan wakizingatia ongezeko la watu wanaohama kutoka vijijini na kuhamia mijini.

Kulingana na Rais Ruto, Kenya pekee inakadiriwa kuwa na vitongoji duni zaidi ya 1,410. Hii ni hali inayohitaji kushughulikiwa kwa umakini na kwa ushirikiano wa serikali za bara zima la Afrika. Vile vile ameweka bayana kuwa kuboresha makaazi ya wananchi ni jukumu la kila kiongozi na serikali katika bara la Afrika.

Kwa upande wake, Waziri wa Arthi, Nyumba, na Maendeleo ya Miji, Zachariah Njeru, amesisitiza umuhimu wa kutumia rasilimali zilizopo kwa njia inayofaa ili kuhakikisha wananchi wasio na uwezo mkubwa kiuchumi wanapata makaazi yanayostahili. Waziri Njeru ameeleza kuwa watu wanaoishi katika vitongoji duni wako katika hatari kubwa ya kuathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi.

 

September 6, 2023