Ruto Kuria

Rais William Ruto amevunja kimya kuhusu gumzo linaloendelea la uhuru wa vyombo vya habari nchini, akisisitiza umuhimu wa pande zote kuheshimu uhuru wa kujieleza.

Akizungumza katika uzinduzi wa mashindano ya Safari Rally huko Naivasha, rais  amesisitiza umuhimu wa kuwaruhusu watu kutoa maoni yao kuhusu mambo yanayokwenda mrama. Aidha, amesisitiza umuhimu wa wanasiasa na viongozi wengine serikalini kutokuingilia utendakazi wa vyombo vya habari.

Rais pia ameitetea kauli ya Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Moses Kuria, akisema kuwa wale wanaohisi wanakandamizwa na vyombo vya habari pia wana haki na uhuru wa kujitokeza na kukosoa vituo vya habari.

Wakati huo huo, maseneta wanaoegemea upande wa Azimio la Umoja walijiondoa kutoka kwa vikao vya leo katika Bunge la Seneti baada ya Spika, Amason Kingi, kukataa ombi lao la kumhoji Waziri Moses Kuria kuhusu matamshi yake ya hivi karibuni kuhusu vyombo vya habari.

Wakiongozwa na Seneta Edwin Sifuna wa Nairobi, viongozi hao wameelezea ghadhabu yao kuhusu hatua ya Waziri Kuria kujitokeza mbele ya Bunge licha ya kuwepo kwa muswada uliowasilishwa tarehe 19 ambao ulipendekeza Waziri huyo ajiwasilishe katika Bunge hilo kwa ajili ya kujibu maswali kuhusu matamshi yake. Sifuna na wenzake wameamua kujitenga na vikao vya leo wakihofia kuwa kuhudhuria vikao hivyo kutampa Waziri Kuria nafasi ya kujitakasa.

June 21, 2023