Kiongozi wa taifa Rais William Ruto amerejea nchini asubuhi ya leo baada ya kukamilisha ziara rasmi katika mataifa ya Italia na Switzerland. Katika ziara hizo, Rais Ruto alihudhuria Mkutano wa Kundi la Nchi Saba Tajiri Duniani (G7) pamoja na Kongamano la Kimataifa kuhusu Amani nchini Ukraine.
Rais Ruto alitua katika Uwanja wa Ndege kwa kutumia ndege ya abiria, ambapo alipokelewa na viongozi wa ngazi za juu serikalini. Miongoni mwa waliomlaki ni Waziri wa Usalama wa Taifa, Prof. Kithure Kindiki, Kiongozi wa Wengi Bungeni, Kimani Ichung’wah, na Seneta wa Kericho, Aaron Cheruiyot, pamoja na viongozi wengine.
Rais Ruto amerudi nchini siku moja kabla ya kuwasilishwa kwa mswada tata wa fedha bungeni hapo kesho Jumanne. Anatarajiwa kufanya mikutano na baadhi ya wabunge ili kujadili na kutafuta uungwaji mkono kwa mswada huo, ambao unaonekana kuwa na umuhimu mkubwa kwa ajenda zake za kiuchumi.