Rais William Ruto ametia saini mswada wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwa sheria katika hafla iliyoandaliwa kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa KICC asubuhi ya leo.
Mswada huo, ambao ulipitishwa na mabunge yote mawili, unatoa mwongozo wa jinsi ya kuwateua maafisa wa tume ya IEBC, ambayo ina jukumu la kuandaa uchaguzi humu nchini. Mswada huu uliandaliwa na Kamati ya Mazungumzo ya Kitaifa ya NADCO.
Sheria mpya itaanza kutekelezwa kwa kuundwa kwa kamati ya wanachama tisa itakayowateua maafisa wa tume ya IEBC. Kamati hiyo itajumuisha:
- Wanachama 2 kutoka Tume ya Huduma za Bunge,
- Wanachama 3 kutoka Kamati ya Vyama vya Kisiasa,
- Mwanachama mmoja kutoka Chama cha Wanasheria Nchini (LSK),
- Mwanachama mmoja kutoka Taasisi ya Wahasibu wa Umma Nchini,
- Wanachama 2 kutoka Baraza la Kidini Nchini.
Kwa sasa, tume ya IEBC haina uwezo wa kutekeleza majukumu yake baada ya makamishna wa tume hiyo kujiuzulu, huku wengine wakistaafu baada ya kukamilisha mihula yao ofisini.