Rais William Ruto ametoa ahadi kuwa hakutakuwa na maandamano ya upinzani nchini juma lijalo. Ahadi hiyo ilitolewa na Rais alipokuwa akizungumza katika eneo la Nakuru baada ya kuzindua barabara ya Njambini kuelekea Naivasha. Rais Ruto alisisitiza kwamba hatavumilia kuandaliwa kwa maandamano siku ya Jumatano kama ilivyotangazwa na viongozi wa upinzani.

Kauli ya Rais ilikujia saa moja baada ya upinzani kutangaza mipango ya kuandaa maandamano kwa siku tatu mfululizo juma lijalo kuanzia siku ya Jumatano. Rais alionekana kutuma onyo kali kwa upinzani, huku akieleza kuwa vurugu zinazotokea wakati wa maandamano hazitaruhusiwa kuendelea tena nchini.

Kauli hii inachukuliwa na wengi kuashiria msimamo thabiti wa Rais dhidi ya maandamano ya upinzani, akielezea azma yake ya kudumisha amani na utulivu nchini, huku sasa wananchi na wadau wengine wa kisiasa wakisubiri kwa hamu kujua hatua zitakazofuata baada ya kauli hii ya Rais Ruto.

 

 

July 14, 2023