Endarasha Hillside Academy

Rais William Ruto ametangaza siku tatu za maombolezi ya kitaifa kufuatia kifo cha wanafunzi 18 wa Shule ya Msingi ya Endarasha Hillside Academy, walioteketea kwenye mkasa wa moto usiku wa kuamkia Ijumaa. Katika taarifa yake ya rambirambi kwa familia za waathirika, Rais Ruto alionyesha huzuni kubwa na kuahidi kuwa serikali itachukua hatua kali kwa yeyote aliyezembea au kuhusika na tukio hilo.

Rais ametangaza kuwa bendera ya taifa na ile ya Afrika Mashariki zitapepea nusu mlingoti katika Ikulu, ofisi zote za serikali, balozi zote za Kenya, na taasisi za ulinzi kuanzia Jumatatu, Septemba 9, hadi Jumatano, Septemba 11, mwaka huu, kama ishara ya heshima kwa wanafunzi waliofariki.

Aidha, Rais Ruto ameahidi kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika wa ajali hiyo ili kuhakikisha tukio kama hilo halitokei tena nchini. Rais aliwahakikishia Wakenya kuwa serikali itaweka mikakati thabiti ili kuzuia majanga kama hayo siku za usoni.

September 7, 2024