Rais Ruto akisalimiana na Gavana Gladys Wanga wa Homabay Baada ya uzinduzi wa Ujenzi wa Barabara za Mfangano.

Rais William Ruto ameendelea na ziara yake katika ukanda wa Nyanza, ambapo leo amezuru kaunti ya Homabay kwa lengo la kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Ziara ya Rais ilianza asubuhi ya leo kwa kuzindua mipango ya uboreshaji wa barabara katika kisiwa cha Mfangano eneo la Sena, kaunti ya Homabay. Ruto aliandamana na gavana wa Homabay, Gladys Wanga, pamoja na viongozi wengine wa kitaifa na wa kaunti.

Katika Hotuba yake, kiongozi huyo wa taifa alitoa wito wa kuendeleza ushirikiano wa karibu kati ya serikali ya kitaifa na ile ya kaunti ya Homabay. Alisisitiza kwamba ushirikiano huu ni muhimu katika kuleta maendeleo kwa wananchi wa Homabay na taifa kwa ujumla. Zaidi ya hayo alisema kwamba ushirikiano ndio njia pekee ya kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inafanikiwa na inawanufaisha wananchi.

SOMA PIA: Rais William Ruto Aanza Ziara ya Siku 4 Nyanza.

Rais pia alisisitiza dhamira yake ya kupeleka maendeleo kila kona ya taifa bila kubagua au kufanya upendeleo. Alionyesha azma ya serikali yake kuhakikisha kuwa kila raia wa Kenya anapata fursa sawa ya kuchangia katika maendeleo ya taifa.

Gavana Gladys Wanga alikaribisha wito wa ushirikiano uliotolewa na rais na kuahidi ushirikiano kufanikisha ajenda ya maendeleo kwa wananchi wa Homabay.

 

 

October 7, 2023