Rais William Ruto ameendelea kutoa wito wa kusitisha mapigano kati ya pande mbili hasimu katika taifa la Sudan. Akihutubia katika mkutano wa mataifa manne ya muungano wa IGAD uliofanyika mjini Addis Ababa, Ruto alisisitiza umuhimu wa jeshi la Sudan na Kundi la Uasi la RSF kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano bila masharti yoyote. Vile vile alisema hatua hiyo itasaidia katika juhudi za kutafuta suluhisho la kudumu kuhusu mzozo unaoendelea nchini Sudan.
Ruto, ambaye alikuwa anaongoza viongozi wa mataifa hayo manne, alieleza kusikitishwa na hali mbaya inayoendelea nchini Sudan, huku akiitaja idadi ya watu waliofurushwa makwao, ambayo imefikia milioni 2.9 hadi sasa, kuwa kubwa zaidi. Muungano wa IGAD umekuwa ukijaribu kuzihusiaha pande zote mbili ili kuleta suluhisho la kudumu kwa mzozo huo.
Kiongozi huyo wa Taifa sasa ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusaidia katika juhudi hizo za amani na kutoa misaada ya kibinadamu kwa watu walioathirika na mzozo huo.
The situation in Sudan is dire: Millions of people have been displaced while lives lost has hit more than 2,000. The intensity and scale of the humanitarian crisis is a harrowing tragedy that calls for a bold and an all-inclusive peace dialogue. pic.twitter.com/UGevdw6R5V
— William Samoei Ruto, PhD (@WilliamsRuto) July 10, 2023
Taifa la Sudan limekumbwa na machafuko ya kisiasa kati ya Jeshi la taifa na jeshi lililoasi la RSF. Pande zote husika zimeshindwa kufikia makubaliano ya kudumu, hali ambayo imepelekea idadi kubwa ya watu kukimbia makwao na kusababisha mzozo wa kibinadamu.