Rais William Ruto pamoja na mawaziri wanatarajiwa kuongoza shughuli za upanzi wa miti katika maeneo mbalimbali ya taifa hii leo. Ruto aliyetangaza likizo ya kitaifa kwa ajili ya zoezi hili, anatarajiwa kuongoza shughuli hizo katika kaunti ya Murang’a.

kiongozi wa taifa aliwahimiza Wakenya kushiriki katika zoezi hili ili kuzuia athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile mafuriko na ukame. Rais alisisitiza kuwa Kenya ina uwezo wa kupanda zaidi ya miti milioni 200 ifikapo mwisho wa siku ya leo.

Naibu wa Rais, kwa upande wake, ataongoza shughuli hizi katika kaunti ya Samburu. Mkuu wa baraza la mawaziri, Musalia Mudavadi, naye anatarajiwa kuongoza upanzi wa miti katika eneo la Chogoria, kaunti ya Tharaka Nithi.

MAWAZIRI KUONGOZA UPANZI WA MITI

Mawaziri wote 22 nchini wanatarajiwa kushiriki katika hafla za upandaji miti katika maeneo mbalimbali ya taifa.

Waziri wa Mazingira, Soipan Tuya, naye ataongoza kampeni hiyo huko Vihiga na Samburu huku waziri wa Usalama wa Ndani, Kithure Kindiki, akitarajiwa kutekeleza shughuli sawia katika kaunti za Marsabit, Mandera, Turkana, Garissa, na Wajir.

Waziri Mithika Linturi wa Kilimo ameratibiwa kuwa katika kaunti za Makueni na Samburu, huku Waziri wa Michezo, Ababu Namwamba, akilenga kuongoza upanzi wa miti milioni moja katika kaunti za Kilifi na Bungoma.

Moses Kuria, waziri wa Utumishi wa Umma, atakuwa katika kaunti za Bungoma, Kisumu, na Siaya naye mwenzake wa elimu Ezekiel Machogu, akiwa Trans Nzoia na Migori.

Eliud Owalo, Waziri wa ICT, atakuwa katika kaunti za Nandi na Kisii, naye waziri wa leba, Florence Bore, akizuru kaunti za Bomet na Nyamira. Zacharia Njeru, Waziri wa Maji, anaelekea katika kaunti za Kajiado na Kiambu kwa shughuli hiyo, huku waziri Alfred Mutua wa Utalii, akiwa Kitui na Taita Taveta.

Waziri wa Uchumi wa baharini Salim Mvurya, atahudhuria kampeni hizi katika kaunti za Tana River na Lamu, huku Waziri wa Jinsia, Aisha Jumwa, akisimamia shughuli hiyo katika kaunti za Kakamega na Kwale.

Aden Duale, Waziri wa Ulinzi, ametumwa katika kaunti za Isiolo na Nakuru na ana lengo la kupanda miti milioni 2.8 kama sehemu ya jitihada za kitaifa za upandaji miti. Mwenzake wa Barabara, Kipchumba Murkomen, atakuwa Homa Bay na Mombasa.

Waziri wa Afya, Susan Nakhumicha, ataongoza wananchi katika shughuli za panda miti katika kaunti za Elgeyo Marakwet na Pokot Magharibi. Simon Chelugui, waziri wa Vyama vya Ushirika, akiwa katika kaunti za Uasin Gishu na Murang’a.

Katika kaunti za Embu na Narok shughuli hizi zitaongozwa na Waziri wa Biashara, Rebecca Miano. Davis Chirchir, waziri wa Nishati, akizuru katika kaunti za Kericho na Baringo, huku Njuguna Ndung’u wa Hazina ya Kitaifa akilenga kuongoza shughuli hiyo katika Machakos na Nyandarua.

Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Peninah Malonza, ataongoza kampeni hiyo katika kaunti za Meru na Busia,. Kwa upande mwingine waziri wa ardhi, Alice Wahome, ataongoza upanzi katika kaunti za Nyeri na Laikipia.

May 10, 2024