Ufa mkubwa umeanza kujitokeza waziwazi kati ya idara ya mahakama na viongozi wakuu serikalini, huku viongozi hao wa kisiasa wakitoa kauli kali dhidi ya maamuzi yanayotolewa na mahakama.
Miongoni mwa viongozi wa hivi karibuni kutoa kauli za kukosoa mahakama ni Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, ambaye ameitaka idara hiyo kutotumiwa kuzuia shughuli za maendeleo nchini. Akizungumza kwenye mazishi ya Mzee Maigo Waweru ambaye ni babake seneta wa Kaunti ya Nyandarua John Methu yaliyoandaliwa siku ya Jumanne katika kaunti ya Nyandarua, Gachagua ameeleza kusikitishwa na hatua za mahakama kusitisha utekelezaji wa miradi ya serikali, akidai kuwa inazuia wakenya kufurahia matunda ya maendeleo.
Rais William Ruto naye hakusita kutoa kauli sawia, akisema maafisa wa mahakama wanaositisha miradi ya maendeleo wanashirikiana na watu wenye nia mbaya dhidi ya serikali. Ruto amesisitiza kwamba tabia kama hii haitavumiliwa nchini Kenya na inaweza kuhatarisha mustakabali wa maendeleo.
Viongozi hao wameonyesha ghadhabu zao mara kadhaa kufuatia maamuzi ya mahakama, hasa baada ya kusitisha utekelezaji wa mipango muhimu kama ujenzi wa Nyumba za bei nafuu na mpango mpya wa bima ya afya.