Rais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA Gianni Infantino, amejibu ukosoaji unaotolewa kwa Qatar kuhusu madai ya ukiukwaji haki za binaadam akisema huu ni unafiki wa mataifa ya Magharibi.
Infantino ameyasema hayo siku moja kabla ya ufunguzi wa mashindano ya Kombe la Dunia hio kesho. Rais huyo amesema kuwa kile kinachoendelea ni unafiki wa hali ya juu, huku akisema kila mmoja anapaswa kuwa huru kumuunga mkono mtu au kundi lolote analolotaka.
Ameongeza kuwa kile Ulaya ilichokifanya miaka 3000 iliyopita inapaswa iwe ikiomba msamaha kwa miaka mingine 3000 Ijayo kabla ya kuanza kutoa ushauri wa maadili kwa watu.
Akizungumza katika mkutano wake na waandishi habari Mjini Doha Infantino ameelezea kuunga mkono watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja na kutambua mchango wa wafanyakazi wa kigeni, pia ametahadharisha kuwa ukosoaji ni muhimu lakini unapaswa kuandamana na suluhisho.