Mkuu wa nchi Rais William Ruto ameanza rasmi ziara yake ya kikazi katika ukanda wa Nyanza asubuhi ya leo. Katika ziara hiyo ya siku nne, rais anatarajiwa kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuongoza katika uzinduzi wa baadhi ya miradi iliyokamilika katika kaunti za Kisumu, Homa Bay, Siaya na Migori.
Rais alianza ziara yake katika eneobunge la Nyando kaunti ya Kisumu, ambapo aliongoza uzinduzi wa ujenzi wa Kituo cha Uvuvi na ukulima wa Maji cha Kabonyo kitakacho igharimu serikali shilingi bilioni 1.
Akizungumza katika hafla hiyo, rais alitangaza kwamba serikali imefutilia mbali deni la viwanda vya sukari katika eneo hilo, kwa nia ya kufufua viwanda hivyo na kuimarisha uzalishaji wa sukari humu nchini.
Kwa upande wake, gavana wa Kisumu Prof. Anyang’ Nyong’o ambaye aliadamana na Rais, alieleza utayari wa serikali ya kaunti yake kupiga jeki juhudi za ukulima wa samaki ili kuimarisha hadhi ya wavuvi katika ukanda huo.
Kabonyo Fisheries and Aquaculture Service and Training Centre, Nyando, Kisumu County. https://t.co/FseAWOwELg
— State House Kenya (@StateHouseKenya) October 6, 2023