Rais William Ruto hii leo ameliongoza taifa kwenye sherehe za siku ya mashujaa ambazo ziliandaliwa katika uga wa Green Stadium mjini Kericho. Wakati wa sherehe hizo rais Ruto amezindua mpango wa afya kwa wote UHC ambapo shehena za dawa zilitumwa kwa kauti mbalimbali humu nchini.

Akitoa hotuba yake wakati wa maadhimisho haya, rais Ruto amesema kuwa kila mkenya ana haki ya kikatiba kupokea huduma bora za afya huku akikumbuka juhudi za serikali iliyopita kufanikisha mpango wa UHC ila hazikufua dafu.

Kuhusiana na suala la kulipwa kwa wahudumu wa afya wa jamii wa kujitolea CHP, rais Ruto amesema kuwa serikali itatenga shilingi bilioni 3 kila mwaka kwa malipo ya wahudumu hao.

Maelfu ya watu walijitokeza kuhudhuria sherehe hizo ambapo.Hafla hii pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo naibu rais Rigathi Gachagua, mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi, jaji mkuu Martha Koome miongoni mwa wengine.

Katika sekta ya elimu Rais  Ruto amesema kuwa suala la uhaba wa walimu litatatuliwa katika miaka miwili ijayo. Akisifia mabadiliko katika sekta ya elimu, rais Ruto ameeleza kuwa walimu 2,000 wa taasisi za kiufundi wataajiriwa ili kufanikisha masomo katika taasisi hizo.

Aidha amesema kuwa Kenya imetia saini mkataba na Uchina kupata vifaa vitakavyosaidia taasisi sabini za kiufundi huku akidokeza kuwa mfumo mpya wa ufadhili wa elimu ya juu umewapunguzia wanafunzi mzigo wa madeni.

 

October 20, 2023