Rais William Ruto amezindua rasmi vifaa vya afya vitakavyotumiwa na wahudumu wa afya wa kijamii, watakaosaidia kukabiliana na matatizo ya kiafya kote nchini.
Mpango huu chini ya mpango wa afya wa UHC, utashuhudia wahudumu wa afya wa kijamii wapatao laki moja wakitumwa katika kaunti zote 47, kusaidia jamii kutambua matatizo ya kiafya kabla hayajaenea zaidi, na kuwawezesha wananchi kupata matibabu kwa muda unaofaa.
Zaidi ya wahudumu 7000 wa kijamii watakaoetekeleza zoezi hili Jijini Nairobi, waliokongamana katika bustani la Uhuru Park mapema leo wanatarajia kupokezwa rasmi vifaa watakavyotumia katika kutekeleza majukumu yao.
Akizungumza kwenye hafla hiyo inayondelea kwa sasa, rais amesisitiza umuhimu wa mpango huu katika kufanikisha ajenda ya serikali, ya kutoa huduma bora za afya, na kuiwezesha serikali kuyajua matatizo ya kiafya yanayohitaji kushughulikiwa ili iweze kuyakabili vilivyo.
Kando na kuwapa vifaa vya usajili na kupima magonjwa mbalimbali, rais ameahidi kwamba serikali itaendelea kushirikiana na serikali za kaunti ili kuwawzesha wahudumu wa afya wa Kijamii kupata malipo kila mwezi ili waweze kuendeleza majukumu yao inavyofaa.
Kwa upande wake naibu wa rais Rigathi Gachagua amewahimiza wakenya kukumbatia mpango huo ambao anasema utapunguza gharama ya matibabu nchini ndani ya miaka mitano ijayo.
Flagging off of Community Health Promoters, #AfyaNyumbani, Uhuru Park, Nairobi. https://t.co/u8qlQSou3o
— State House Kenya (@StateHouseKenya) September 25, 2023