Ofisi za wachumba wa rais, naibu wa rais na mkuu wa mawaziri hazitaendelea kupokea mgao wa fedha kutoka kwa bajeti ya kitaifa. Haya yametangazwa na rais William Ruto.
Akilihutubia taifa katika ikulu ya Nairobi, rais Ruto ameeleza kuwa hatua hii inanuia kupunguza matumizi ya serikali ikizingatiwa kuwa mswada wa fedha wa mwaka 2024 ulitupiliwa mbali.
Mabadiliko haya pia yanajiri kufuatia shinikizo kutoka kwa umma kwamba ofisi hizo zitupiliwe mbali kwani haziko kwenye katiba.
Aidha sio tu ofisi hizi ndizo zimeathirika kufuatia msururu wa mabadiliko ambayo yametangazwa na rais. Mabadiliko mengine ambayo yatatekelezwa mara moja ni pamoja na kupigwa marufuku kwa maafisa wa serikali kuchangisha fedha kwenye mikutano ya hadhara, kupunguzwa kwa idadi ya washauri kwa asilimia 50 katika tume ya utumishi wa umma, kuahirishwa kwa mchakato wa kuwaajiriwa kwa makatibu waandamizi miongoni mwa mabadiliko mengine.
Press Briefing, State House, Nairobi. https://t.co/rJD76poqUU
— William Samoei Ruto, PhD (@WilliamsRuto) July 5, 2024