Rais William Ruto anatarajiwa kuondoka nchini kuhudhuria Kongamano la umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya Tabia nchi almaarufu COP 28 huko Dubai. Ruto, ambaye amekuwa kiongozi wa Afrika katika wito wa kuchukuliwa hatua za hali ya hewa, atakuwa akitetea Kenya na ajenda ya hali ya hewa ya bara hili katika nafasi yake kama Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali za Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.
Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed anasema katika taarifa kwamba rais Ruto anapania kusisitiza hatua za mabadiliko ya hali ya hewa zinazohitajika haraka ili kurekebisha hali ya sasa ya ulimwengu.
Pia atatoa taarifa kwa niaba ya Afrika, akiangazia vipaumbele vya bara hili huku akiendeleza Azimio la kihistoria la Viongozi wa Afrika la Nairobi lililopitishwa katika Mkutano wa kwanza wa Kilele wa Hali ya Hewa Afrika uliofanyika Nairobi Septemba 2023.
Wakati huo huo, hafla ya ufunguzi rasmi wa kongamano hilo la COP 28 limefanyika hii leo nchini Dubai. Kauli mbiu ya mwaka huu ni kubadili matumizi ya kawi kwa mataifa ili kukumbatia kawi isiyochafua hewa.
Hata hivyo baadhi ya wanaharakati wa mazingira wamejitokeza na kusisitiza kwamba mataifa yaliyoendelea yaweze kutekeleza ahadi walizotoa wakati wa kongamano kama hili mwaka jana hususan ufadhili wa fedha ili kusaidia mataifa maskini kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi