Rais William Ruto amewasimamisha kazi makamishna wanne wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC wanaotuhumiwa kwa utovu wa nidhamu na ukiukaji wa Katiba.
Wanne hao ni pamoja na naibu mwenyekiti wa IEBC Juliana Cherera, Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyang’aya.
Kusimamishwa kwao kunafungua njia ya uchunguzi kuhusu mienendo yao na jopo la wanachama tisa baada ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 9 yaliyotangazwa na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati.
Makamishna hao wanne walimshtumu Chebukati kwa kubadilisha matokeo na kumpendelea Rais William Ruto, na hivyo kumnyima kura mshindani mkuu wa Ruto Raila Odinga.Kamati ya Bunge ya Kitaifa ya Haki na Masuala ya Kisheria (JLAC) ilikuwa imependekeza kwa rais kuunda jopo la kuchunguza wanne hao kuhusu mienendo yao.
Rais ameliagiza jopo hilo kuharakisha uchunguzi na kuwasilisha ripoti yake kwake.Jopo hilo linaweza kupendekeza kufutwa kazi kwa makamishna hao au kurejeshwa kazini kikamilifu.
Kwa sasa makamishna hao hawataruhusiwa kutekeleza majukumu yao, lakini watalipwa nusu ya mishahara yao ya kila mwezi.