Kuwasilishwa kwa ripoti ya kamati ya Mazungumzo

Kiongozi wa Taifa, Rais William Ruto, amepokezwa ripoti ya Kamati ya Mazungumzo ya Kitaifa katika katika Ikulu ya Nairobi siku ya Ijumaa. Viongozi wa kamati hiyo ya mazungumo ya kitaifa wakiongozwa na Kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichungwa na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka ndio waliiwasilisha ripoti yenyewe.

Ripoti hii iliandaliwa kufuatia mazungumzo ya kitaifa yaliyoongozwa na viongozi wa Muungano wa Kenya Kwanza na wale wa mrengo wa Azimio la Umoja. Ripoti hiyo, ambayo tayari imewasilishwa bungeni, inajumuisha mapendekezo mbalimbali ya utekelezaji wa mambo muhimu nchini, ikiwa ni pamoja na suala la uundaji wa Tume ya Uchaguzi IEBC na utekelezaji wa sheria ya thuluthi mbili ya jinsia.

Katika hotuba yake, Rais Ruto ameipongeza pande zote mbili kwa ushirikiano wao katika kufikia makubaliano muhimu yanayohusu mustakabali wa Kenya.


Katika hafla tofauti, ripoti hiyo imekabidhiwa pia kwa Kinara wa muungano wa Azimio Raila Odinga, ambaye amesisitiza kwamba mapendekezo yaliyo katika ripoti hiyo yatasaidia Kenya kufanya maendeleo makubwa kimaendeleo na kidemokrasia.

Pamoja na hayo, Odinga ameeleza azma ya muungano wa Azimio la Umoja kuendelea kushinikiza serikali kuboresha gharama ya maisha kwa wananchi, licha ya suala hilo kutokuwa sehemu ya mazungumzo yaliyojumuishwa kwenye ripoti ya mwisho.

 

March 8, 2024