Waziri wa kawi nchini Opiyo Wandayi amesema kuwa ripoti ya Marekani kuhusu kampuni ya adani kwamba walitumia ulaghai kupata mkataba, haitaathiri kwa namna yoyote kandarasi ya umeme kati ya Kenya na kampuni hiyo.

Akizungumza alipofika mbele ya kamati ya kawi katika bunge la kitaifa, Wandayi amesema kwamba walifanya uchunguzi wa kina na kufuata mchakato hitajika kabla ya kutia saini mkataba wowote.

Alisema kuwa ofisi ya mkurugenzi wa PPP, kwa kushirikiana na KETRACO, ilifanya zoezi la uhakiki mkali kwa Adani katika awamu mbili ambazo zilithibitisha kuwa walikuwa wanafaa kukabidhiwa kandarasi hiyo.

Kwa hivyo, Waziri Wandayi alibaini kuwa kesi ya mashitaka ambayo Adani inakabiliana nayo nchini Marekani haitalemaza mpango wa nishati nchini Kenya kwa sababu madai ya hongo hayajatolewa wakati KETRACO ilipotoa mwanga kwa kundi hilo.

Katika mpango wao na Kenya, Adani itasimamia laini za usambazaji umeme na vituo vidogo itakavyojenga kwa miaka 30, na kisha mradi huo na mali zake zote zitakabidhiwa kwa KETRACO “katika hali nzuri na bila vizuizi vyovyote.”

November 21, 2024