Serikali imetoa wito kwa wakenya kujikaza na kujiandaa kukabiliana na changamoto za kiuchumi zinazowakabili katika siku zijazo. Mkuu wa Baraza la Mawaziri, Musalia Mudavadi, ameeleza kwamba serikali inahitaji muda zaidi kabla ya kurejesha gharama ya maisha katika viwango vinavyokubalika.

Akitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa kongamano la ujasiriamali katika Kanisa la ACK St. Marks huko Westlands, Mudavadi alisisitiza umuhimu wa subira na uvumilivu katika kufikia mafanikio ya kiuchumi.Aidha waziri huyo aliweka wazi kuwa serikali itahitaji angalau miaka miwili na nusu ili kutekeleza mikakati yake ya kupunguza gharama ya maisha nchini.

Mudavadi alibainisha kuwa serikali itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza nafasi za ajira na kuimarisha uchumi, ili kuinua kiwango cha maisha cha Wakenya. Pia alisisitiza umuhimu wa kujenga mazingira bora kwa wajasiriamali na kuvutia uwekezaji, ambayo yatachangia ukuaji endelevu wa uchumi na ustawi wa wananchi.

June 23, 2023