Serikali ya kaunti ya Narok imetoa jumla ya shilingi 579,280 kwa Wanafunzi 16 ambao ni walemavu ili kufanikisha ndoto yao ya elimu kupitia ofisi ya watu wanaoishi na ulemavu kaunti ya Narok.
Akizungumza mjini Narok mkurugenzi wa watu wanaoishi na ulemavu kaunti ya Narok Julius Ntayia amesema hatua hiyo inalenga kufanikisha ndoto ya wanafunzi hao hadi vyuo vikuu nchini.
Ntayia ameshabikia hatua ya ofisi ya kamishana wa kaunti ya Narok kuwasaidia wanafunzi wanaoishi na ulemavu kila wakati bila kusita.
Kamishana wa kaunti ya Narok Isaac Masinde kwa upande wake ametoa wito kwa wale wanaowaficha watoto walemavu kuwapeleka shuleni ili kuhakikisha wamepata elimu bila ubaguzi.
Kamishana huyo amedokeza kuwa ofisi yake itashirikiana na Machifu na manaibu wao kufanikisha hatua hiyo na kuwaonya wale wanaokiuka sheria na haki ya watu wanaoishi na ulemavu.
Wazazi wa wanafunzi hao wameelezea furaha yao na kuishukuru ofisi hiyo kwa kutoa fedha hizo ambazo wamesema zitawasaidia pakubwa.
Aidha wameitaka serikali kuhakikisha kuwa wanafunzi walemavu wamepewa ulinzi wa kutosha ili kuzuia dhuluma na unyanyasaji.