Angata Barrikoi

Gavana wa Kaunti ya Narok, Patrick Ntutu, ameitaka Mamlaka ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA) kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusu mauaji ya watu sita yaliyotokea katika eneo la Angata Barrikoi, Jumatatu tarehe 28 Aprili 2025.

Kupitia taarifa rasmi aliyotoa kwenye mitandao ya kijamii, Gavana Ntutu alisema alitembelea eneo la tukio jana jioni. Lengo lake lilikuwa kutathmini hali halisi na kuwapa pole familia za waathiriwa pamoja na wakazi wa Angata Barrikoi. Tukio hilo la kusikitisha linahusishwa na mzozo wa ardhi kati ya maeneo ya Angata na Moyoi. Mzozo huo ulikuwa karibu kutatuliwa baada ya zaidi ya mwaka mmoja na nusu wa usimamizi wa serikali ya kaunti.

Ili kusaidia waathiriwa, serikali ya kaunti ya Narok itatoa msaada kamili kwa ajili ya mazishi ya wote waliopoteza maisha, akiwemo mtoto wa miaka saba. Vilevile, serikali hiyo imeahidi kugharamia matibabu ya wote waliojeruhiwa.

Wakati wa ziara hiyo, Gavana Ntutu aliandamana na viongozi mbalimbali. Walikuwepo Mbunge wa Emurua Dikirr, Johana Ngeno, Kamishna wa Kaunti ya Narok, Kipkech Lotiatia, na Kamanda wa Polisi wa Kaunti, Ngare. Hii ilikuwa ni ishara ya mshikamano wa serikali katika kushughulikia hali hiyo.

Kwa upande mwingine, Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, alitangaza kuwa serikali imeimarisha usalama katika eneo hilo. Aliwahimiza wakazi kudumisha utulivu na kuepuka vitendo vya ghasia.

Aidha, Gavana wa Kaunti ya Bomet, Hillary Barchok, alilaani vikali mauaji hayo. Alieleza masikitiko yake kutokana na vifo vilivyotokea na akatoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa haki ili waathiriwa wapate haki wanayostahili.

April 29, 2025

Leave a Comment