Gavana wa kaunti ya Narok Patrick Ole Ntutu ameahidi kufanya ujenzi wa kiwanda cha maziwa katika kaunti ya Narok kwa lengo la kuwawezesha wananchi wa Narok na hasa wafugaji kunufaika na maziwa ya mifugo wao.
Ntutu akizungumza katika eneo la Sikinani Narok magharibi amesema kwamba kaunti ya Narok ni miongoni mwa kaunti ambazo zinachangia asilimia kubwa ya maziwa humu nchini, lakini ni jambo la kughadhabisha kuona kwamba wafugaji hawajakuwa wakinufaika kupitia biashara hiyo ya maziwa. Gavana huyo ameshikilia kwamba serikali yake itaangazia ujenzi wa kiwanda cha maziwa ambapo wafugaji watakuwa wanapeleka maziwa yao kule kuuza kwa bei bora na hapo kujiimarisha kiuchumi kupitia biashara hiyo. Amesisitiza kwamba mtindo wa wenyeji wa Narok kupeleka maziwa yao kutafuta soko nje ya kaunti hii itaisha pindi tu kiwanda hicho kitakapojengwa.