BY ISAYA BURUGU 29TH NOV 2023-Serikali imekanusha  madai kwamba watoto wachanga watapandikizwa vibandiko vya kielektroniki mwilini mwao katika ugavi wa vitambulisho vya kidijitali.

Katibu Mkuu wa Uhamiaji na Huduma kwa Raia Prof Julius Bitok, katika taarifa yake kwa vyumba vya habari, aliondoa hofu akisema kuwa habari hizo potofu ni propaganda za  kampuni za kigeni baada ya serikali kuwanyima kandarasi za biashara katika uhamiaji wa vitambulisho vya kidijitali.

Bitok, ambaye alikuwa akihutubia Baraza la Maaskofu Katoliki  nchini  (KCCB) katika Jumba la Waumini House baada ya wito wa kufafanua ripoti hizo, alipuuza madai hayo kama ushindani wa kibiashara wa makampuni ya kimataifa ambao haujafurahishwa na uamuzi wa serikali wa kuharakisha mradi huo.

Prof. Bitok alitetea uamuzi wa kuzingatia masuluhisho ya teknolojia ya habari ya nyumbani katika uhamishaji wa kidijitali kwa wasiwasi kuhusu ulinzi na uadilifu wa data na hivyo makampuni ya kigeni hayangeweza kukabidhiwa jukumu la kutekeleza mradi huo.

Baraza la maaskofu katoliki nchini  ilikuwa imeibua wasiwasi kuhusu madai ya kupandikizwa kwa vibandiko na maswala mengine yaliyoonekana kuzungukwa na wingu jeusi kuhusu  kitambulisho cha kidijitali na kuitaka serikali kuangazia suala hilo.

Maaskofu waliozungumza mjini Nakuru pia walitoa wito wa ushiriki zaidi wa umma na ushiriki wa washikadau katika utoaji wa vitambulisho vya kidijitali.

 

November 29, 2023