Waziri wa usalama Kithure Kindiki hii leo amezuru kaunti ya Garissa ambapo amefanya mkutano na wakuu wa usalama pamoja na maafisa wa kupambana magaidi baada ya kufunguliwa tena kwa mpaka wa Kenya na Somalia.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Kindiki ameeleza kuwa serikali inakusudia kufungua upya afisi za uhamiaji za Kanda ya Mashariki huko Garissa katika juhudi za kuwezesha usindikaji wa haraka wa hati muhimu akidai kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za utawala wa Kenya Kwanza kuimarisha upatikanaji sawa wa huduma bora.
Katika jitihada za kuongeza uwezo wa timu maalumu za ulinzi na kijasusi nchini kupambana na ugaidi na uhalifu mwingine unaohusiana na hayo, Kindiki alisema serikali itawekeza shilingi bilioni 20 katika uboreshaji wa vifaa vya usalama.
Uboreshaji wa kisasa ambao utaona upatikanaji wa ndege za kisasa na silaha za moto pamoja na ujumuishaji wa teknolojia za kisasa unakusudiwa kusaidia nchi kukabiliana ipasavyo na matishio ya usalama ya kisasa kama vile ugaidi, uhalifu wa kuvuka mipaka, ujambazi na wizi wa mifugo, biashara ya pombe haramu, madawa ya kulevya na vitu vya kisaikolojia.
Aliandamana na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Noor Gabow, viongozi wa kidini, wajumbe wa Kamati za amani za kanda, Gavana wa Garissa Nadhif Jama pamoja na viongozi wengine wa kisiasa kutoka kanda hiyo.