Serikali imepiga marufuku na kusitisha shughuli za usajili wa wakenya katika sarafu mpya ya kidijitali ya World Coin. Hatua hii imetangazwa na Waziri wa Usalama wa Ndani nchini, Kithure Kindiki, katika chapisho lake la asubuhi ya leo.

Uamuzi wa kusitisha usajili huo umetokana na wasiwasi wa serikali kuhusu matumizi mabaya ya taarifa za wakenya chini ya mpango huu. Kwa sasa, uchunguzi umeanzishwa mara moja ili kubaini uhalali wa usajili huo. Shughuli za usajili zitarejelewa baada ya idara husika kupata kibali cha kusonga mbele na zoezi hilo.

Mpango wa sarafu za World Coin unaendeshwa na kampuni ya Marekani na tayari umewasajili maelfu ya wakenya, ambao wamepokea shilingi elfu saba, baada ya kutambazwa kwa mboni ya jicho lao. Hata hivyo, kutokana na hatua hii ya serikali ya kusitisha usajili huu, onyo limetumwa kwa yeyote atakayejihusisha na usajili huo kuwa atakabiliwa na hatua kali za kisheria.

 

August 2, 2023