BY ISAYA BURUGU 2ND SEPT 2023-Jumla ya watu 1,699,759 wamepokea chanjo ya kipindupindu tangu Agosti 3 ilipozinduliwa kampeni ya chanjo ya Oral Cholera (OCV) inayolenga kaunti nane zilizo katika hatari kubwa ambapo milipuko ya ugonjwa huo imeripotiwa mara kwa mara.
Katika taarifa yake kwa vyumba vya habari Jumamosi, Katibu Mkuu wa Afya ya Umma (PS) Mary Muthoni amebainisha kuwa idadi ya watu waliopata chanjo imepita kiwango kilicolengwa awali cha watu 1,590,378, ikiashiria kiwango cha chanjo cha asilimia 104.5.
PS aliongeza kuwa Wizara ya Afya itaendelea na kampeni ya chanjo katika mwaka mzima wa 2024 huku akibainisha kuwa Kenya imekamilisha Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Kipindupindu kuelekea kumaliza ugonjwa huo ifikapo 2030.
Alibainisha zaidi kuwa kampeni tofauti ya kupambana na polio, iliyoanzishwa katika kaunti nne kuanzia Agosti 24-28, ilisababisha chanjo ya watoto 1,957,476 walio na umri wa chini ya miaka mitano, na kufikia kiwango cha chanjo cha asilimia 104.2.