BY ISAYA BURUGU,27TH NOV 2023-Takriban Wakenya 76 wameuawa na mvua inayoendelea ya El Nino ambayo imesababisha maafa kote nchini kutokana na mafuriko, maporomoko ya udongo na majanga yanayohusiana nayo.

Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed amesema kuwa Baraza la Mawaziri, katika kikao cha dharura hivi leo  kilichoongozwa na Rais William Ruto kilikuja na hatua kadhaa za kusaidia kupunguza athari za El Nino kwa Wakenya.

Haya yanajiri kufuatia mafuriko ambayo yamesababisha vifo vya watu, familia kuhama na kuharibu mali.Msemaji wa Ikulu pia alibaini kuwa serikali imetenga Ksh.7 bilioni kushughulikia athari za mvua.Sehemu ya pesa hizo, Bw Mohamed alisema, ni za wafugaji wa ng’ombe wa maziwa huku serikali ikichukua hatua ya kununua maziwa ya ziada.

Mohamed pia aliorodhesha barabara, madaraja na uwanja wa ndege ambao umefanyiwa ukarabati baada ya kuharibiwa na mvua kubwa na mafuriko.Pia alisema kuwa kamati ya dharura ya Baraza la Mawaziri iliundwa kuhusu kukabiliana na majanga itakayoongozwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua.

November 27, 2023