BY ISAYA BURUGU,13TH NOV,2023-KATIBU katika Wizara ya Afya Mary Muthoni amehimiza magavana kuajiri wahudumu zaidi wa afya zaidi ili kupunguza uhaba unaoshuhudiwa katika vituo vya afya nchini.
Kulingana na Bi Muthoni, uchunguzi wa serikali ya kitaifa unaonyesha kuwa hospitali nyingi zina wafanyikazi wachache, licha ya kuwa ni jukumu ya kila serikali ya kaunti kuhakikisha kuwa vituo vyao vina wafanyikazi tosha.
Chini ya Katiba ya sasa iliyopitishwa na kuidhinishwa 2010, Sekta ya Afya imegatuliwa magavana wakipaswa kuiwajibikia.
Katibu Muthoni alisema kuwa kuajiri wafanyakazi wengi, kutasaidia kukidhi mahitaji ya idadi ya watu wanaotafuta huduma za afya.
Alisema hayo baada ya kukutana na wanawake katika eneo la Nkoben, Kaunti Ndogo ya Narok Kusini, Kaunti ya Narok.
“Tumezuru hospitali zote nchini na tumegundua kwamba kuna hitaji la wafanyikazi zaidi kwa sababu serikali za kaunti zina majukumu ya kuajiri madaktari na wauguzi ili wahudumie wananchi,” Bi Muthoni alisema.
Hata hivyo, aliwaomba Wakenya kutembelea vituo vya afya mara kwa mara ili wapate uchunguzi na kukaguliwa ugonjwa hatari wa Saratani akisema hatua hiyo itasaidia madaktari kuugundua mapema kwa minajili ya matibabu.
Akihutubia wanawake hao, alisema ni muhimu watu kushiriki hafla za uhamasishaji Kansa (Saratani) kwa sababu wataelewa umuhimu wa kaguzi za mara kwa mara.
Katibu huyo alimpongeza Rais William Ruto kwa kutia saini miswada minne kuwa sheria ambayo itaboresha afya ya Wakenya.
Pia alifichua kuwa serikali inapania kuendesha mchakato utakaochukua data ya wafanyikazi wa matibabu kote nchini, ili kuweza kubaini pengo lilipo.