Mahakama ya kutatua migogoro ya maswala ya kisiasa nchini imesitisha uamuzi wa kubanduliwa kwa seneta wa kaunti ya Isiolo Fatuma Dullo kama mnadhimu wa walio wachache katika bunge la seneti.
Naibu Spika wa Bunge hilo Kathuri Murungi, ameeleza kwamba amepokea tangazo kutoka kwa mahakama hiyo ya kutatua mizozo ya kisiasa kusitisha uamuzi wa muungano wa Azimio hadi pale uamuzi kuhusiana na suala hilo utakapotolewa.
Juma lililopita, kinara wa muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga, alitangaza kuondolewa kwa Seneta huyo wa Isiolo katika wadhifa wake na kutwaliwa na Seneta wa Narok Ledama Ole Kina.
Katika kikao cha alasiri ya leo kwenye bunge hilo, seneta Abdulkadir Haji, alieleza kwamba chama cha Jubilee bado ni mwanachama wa Azimio na kuwa hawatakubali kudhulumiwa wakiwa ndani ya chama chao. Aidha aliweka wazi kwamba tofauti Iliyomo katika muungano huo ni wa mtazamo wala sio misimamo yao bungeni.