BY ISAYA BURUGU 12TH JULY 2023-Shughuli za kawaida zimetatizika pakubwa haswa katika Barabara nyingi nchini huku magari machache yakionekana katikati mwa jiji la Nairobi leo asubuhi kufuatia taharuki iliyochangiwa na maandamano yaliyoitishwa na muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya na mgomo wa madereva wa magari.
Kufikia mwendo wa moja na nusu asubuhi, barabara za Moi Avenue, Kimathi Street, na barabara ya Koinange miongoni mwa nyingine zimekuwa na idadi ndogo zaidi ya magari.
Hata hivyo, kumekuwa na magari machache ya matatu katika baadhi ya vituo vya matatu Khoja, Tea Room, OTC barabara ya Tom Mboya na Ronald Ngala.Polisi walionekana wakishika doria katika baadhi ya barabara kadhaa za Nairobi wakilinda doria kuhakikisha kuwa waandamanaji hawafiki hawaingii katikati mwa jiji.Maduka mengi yalikuwa yamefungwa majira ya asubuhi, wenyewe wakihofia hasara kutokana na makabiliano kati ya polisi na waandamanaji.
Aidha Radio Osotua imebaini kuwa baadhi ya wanafunzi hawakuenda shuleni baada ya wasimamizi wa shule hizo kuwashauri wasalie nyumbani.Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome ameshatangaza marufuku maandamano yaliyopangwa na Azimio katikati mwa jiji na maeneo mengine nchini.
Wakati huo huo maafisa wa polisi wamekabiliana na vijana waliokuwa wakiandamana katika Barabara kadhaa jijini Kisumu.Barabara za kutoka Kakamega na kuingia jijini zimewekwa vizuizi sawa na ile ya kutoka Busia mjini kuelekea Kisumu eneo la Otonglo.
Hata hivyo eneo la Kondele ndilo lililoshuhudia utata huku vijana wakizuia magari kungia jijini huku wale wlaio na nia ya kuingia wakitakiwa kutoa kiasi Fulani cha pesa.Tofauti na hali ambapo moto huwashwa barabarani,
leo vijana hao hawakuwasha moto.Maafisa wa polisi pia wanaonekana wakikitaka kambi katika maeneo tofauti jijini Kisumu.
Katika jiji la Mombasa wandamanaji wamefanya mazungumzo na maafisa wa polisi huku wakielezea masaibu wanayopitia maishani na wakitaka polisi kuwaruhusu kuwasilisha malalamishi yao katika afisi ya kaunti kamishna.Wandamanaji hao walioapa kutozua fujo wamesema polisi wanafaa kuwaruhusu kuendelea na mandamano yao kwa njia ya Amani kwani wameruhusiwa kikatiba
.
Tusalie na taarifa inayofungamana na hiyo ambapo maafisa wa polisi wamekabiliana na wandamanaji jijini Nakuru huku wakilazimika kurusha vitoa machozi kuwatawanya.Katika makabiliano hayo wandamanaji watatu wametiwa mbaroni. Kufikia wakati wakuchapisha taarifa hii, maandamano yameshuhudiwa Kisii, Nyamira, Migori, Kisumu, Nairobi na Nakuru.
Kwa upande wa Nyeri, ambayo ni ngome ya Naibu Rais Rigathi Gachagua, madereva wa magari pia waliingia barabarani kuandamana.Wengi walilalamika kwamba walihitaji malalamishi yao kushughulikiwa.Pia, baadhi ya waendeshaji matatu walisimamisha shughuli.