Shughuli za masomo katika shule ya upili ya Mukumu Kaunti ya Kakamega zimesitishwa baada ya shule hiyo kufungwa kwa muda usiojulikana kufuatia maradhi yaliyowaandamana wanafunzi shuleni humo na kusababisha kuaga dunia kwa wanafunzi wawili.
Inakisiwa kwamba wanafunzi hao walikula chakula kilichokua kimeathirika, baada ya wengi wa wanafunzi kuanza kulalamika kuhusu maumivu ya tumbo na kusababisha Zaidi ya wanafunzi 200 kupekelekwa hospitalini. Mkurugenzi wa Elimu katika ukanda wa Magharibi Jared Obiero, ambaye aliitembelea shule hiyo mapema leo, ametangaza hatua ya kufungwa kwa shule hiyo huku wizara ya Afya ikianzisha uchunguzi ili kubaini kilichosababisha hali hiyo.
Aidha seneta wa kakamega Boni Khalwale amenyooshea usimizi wa shule hiyo kidole cha lawama, akisema walizembea katika jukumu lao la kuitunza afya ya wanafunzi hao. Khalwale ameeleza kwamba hatua za kisheria zinafaa kuchukuliwa dhidi ya usiamizi wa shule hiyo, huku akiahidi msaada wa serikali ya kaunti kwa jamaa za walioathirika.