Kinara wa muungano wa Umoja Raila Odinga ametoa ahadi ya kuzidi kushirikiana na viongozi wenza wa muungano wa Azimio, hata endapo atachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Muungano wa Afrika (AU). Kwenye hotuba yake kwa viongozi, wawekezaji, na wageni waliohudhuria kongamano la kimataifa la uwekezaji katika Kaunti ya Homa Bay, Odinga amesisitiza azma yake ya kubaki na kujikita katika masuala ya ndani ya nchi huku akiendelea kusaka uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wa Afrika.
Odinga ameeleza kwamba licha ya jitihada zake za kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wa mataifa mbalimbali barani Afrika, kama vile Namibia na Uganda, ataendelea kuwa mwangalifu kuhusu masuala ya ndani ya Kenya na kufanya kila awezalo kwa faida ya wakenya.
Hata hivyo Kinara huyo wa Azimio, amekanusha uvumi uliosambaa kuhusu ziara yake na Rais William Ruto nchini Uganda kuwa ilikuwa imepangwa. Odinga ameeleza kuwa lengo la ziara yake na Rais Museveni ilikuwa kutafuta uungwaji mkono kwenye azma yake ya kuwania uenyekiti wa AU, wakati Rais Ruto alifanya ziara hiyo kwa ajili ya kujadili masuala ya usafirishaji wa mafuta kati ya Kenya na Uganda.