Wito umetolewa kwa wazazi kuendeleza mahusiano ya karibu na wana wao ili kuwaongoza katika njia inayofaa. Vilevile njia hii imetajwa kama itakayosaidia kukabiliana na matatizo mbalimbali ya maisha, ikiwemo suala la dawa za kulevya. Wito huu umetolewa na Bi. Jane Sankok, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Ilmashariani Mjini Narok, aliyezungumza katika siku ya kuwasherehekea walimu ulimwenguni.
Bi. Sankok amesisitiza umuhimu wa wazazi kuwa karibu na wana wao, akibainisha kuwa uhusiano wa karibu unaweza kusaidia kuzuia na kutatua changamoto za kijamii zinazowakabili vijana wa leo. Amesema kuwa wazazi wanapaswa kutekeleza jukumu lao la ulezi kwa ushirikiano, na sio kuwaachia wakufunzi hawa majukumu yote ya kuwalea watoto.
Kauli hii imeungwa mkono na Askofu Augustine Rugut wa Kanisa la Gospel Power, ambaye ameonyesha wasiwasi wake kuhusu hali ya elimu na malezi nchini. Askofu Rugut amehimiza serikali kutambua mchango wa mwalimu na kuimarisha utendakazi wake. Vile vile ameeleza umuhimu wa kuwapandisha vyeo wale waliofanya vyema katika shule mbalimbali badala ya kuwapatia uhamisho.
SOMA PIA: Kenya yaungana na ulimwengu kuadhimisha siku ya walimu.
Wakati hayo yakijiri, vyama vya kutetea maslahi ya walimu vimeshinikiza malipo bora kwa wanachama wake. Katibu Mkuu wa KUPPET Akello Misori, na mwenzake wa KNUT Collins Oyuu, wamesisitiza kuwa ni muhimu kwa Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) kutoa maslahi bora kwa walimu, haswa ikizingatiwa changamoto zinazowakumba.
Wanashinikiza kuboreshwa kwa mazingira ya kazi, na malipo ya haki ili kuwapa motisha na kuimarisha ubora wa elimu nchini.
Siku ya Walimu Duniani ni siku ya kimataifa inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Oktoba kusherehekea kazi ya walimu. Siku hii ilianzishwa mwaka 1994.